Miaka 46 ya Uhuru!

Mama Salma Kikwete akipokea Mwenge wa UhuruWatanzania wanasheherekea jambo gani, na wana sababu gani ya kusheherekea?

 

TAREHE 9 Desemba ya kila mwaka, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi wake, huadhimisha siku ambayo nchi hii ilipata ‘uhuru’ wake kutoka kwa watawala wa kikoloni. Tarehe 9 Desemba 1961, Jamhuri ya Tanganyika ilizaliwa, baada ya jitihada za muda mrefu za waasisi wa nchi hii kutumia mbinu mbali mbali kuwashawishi watawala wa kikoloni wa Uingereza, kuipa ‘uhuru’ nchi hii.

Baadhi ya wanahistoria wanasema kwamba ‘uhuru’ wa nchi hii ulipatikana bila kumwaga damu, lakini baadhi ya wanahistoria wanasema pia kwamba wapo Watanganyika waliojitolea uhai wao kupigania ‘uhuru’ wa nchi yao. Hao ni wale ambao waliamini kwamba amani na uhuru ndani ya nchi yao isingepatikana ila kwa ncha ya upanga, na ni wale ambao waliingia misituni kujipanga kivita, iwapo jitihada za kudai uhuru bila kumwaga damu – kwa wingi – zisingefanikiwa. Hata hivyo, wachache hawa, katika harakati zao za kutafuta amani, baadhi yao walipoteza roho zao; Siku ya Mashujaa inawakumbuka daima, ingawa hawatajwi rasmi… wanaotajwa ni wale ambao walipigana kwenye Vita Kuu ya Pili, wakati ambapo tulikuwa chini ya utawala wa kikoloni.

Si kusudio ya makala haya kuzungumzia jitihada za kutafuta ‘uhuru’ wa Tanganyika, ambayo hatimaye ilibadilika na kuwa Tanzania baada ya muungano na Zanzibar. La hasha. Kusudio la makala haya ni kudadisi endapo Watanzania wanasheherekea jambo gani, kila nchi hii inapoadhimisha siku hiyo ambapo nchi yao ilizaliwa rasmi, au endapo wana sababu ya kusheherekea.

Daima mimi ni ‘mchokozi’ wa mada, kwani katika kuchokoza mada hizi kutoka kwa wananchi wenzangu, ninapata upeo mkubwa zaidi wa jinsi ambavyo Watanzania wenzangu wanafikiria, kuhusu mustakabali wao kisiasa, kijamii na kiuchumi. Katika kuchokoza mada hii, nimegundua mambo mazito ambayo, nina hakika yatawachefua baadhi ya walengwa wanaotajwa na Watanzania wenzangu. Daima, ukweli unauma, lakini mimi ni mjumbe, nimetumwa na Watanzania wenzangu, nipeleke ujumbe kunakostahili. Mjumbe hauwawi….

Katika maudhui ya ‘uhuru’ wa Tanzania, makala haya yanadadisi na kutoa tafakuri na maono ya wananchi wa kawaida, kuhusu mustakabali wa Watanzania, kisiasa, kijamii na kiuchumi, kama ifuatavyo.

Kisiasa: Watanzania wengi wamekiri na kutambua kwamba himaya ya kisiasa nchini mwao, toka enzi za chama kimoja hadi sasa, ilikuwa, ipo na itaendelea kuwa chini ya udhibiti wa kikundi kimoja cha Watanzania, ambao wamebatizwa jina la ‘wakoloni weusi’. Haya ni maoni ya baadhi ya Watanzania – wa hali ya kawaida kabisa – waliotoa maoni yao kwenye mitaa kadhaa ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya kuhojiwa na mwandishi wa makala haya. Watanzania hawa wamesema kwamba ‘wakoloni weusi’ hawa wamekuwa ‘wakiwazuga’ Watanzania walio wengi, kwa vishawishi kadhaa, kila ufikapo wakati wa uchaguzi mkuu, kwa kuwapa zawadi za ‘kinafiki’, pamoja na kutoa ahadi lukuki ambazo hazitekelezwi kamwe. Kwa masikitiko, Watanzania hao – ambao ni wale wenye unafuu wa kuweza kumudu gharama za kuishi kwenye miji mikubwa, japo kwa shida – wamesema hawana imani kwamba sera ya ‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania’, ambayo ndiyo iliyokuwa kaulimbiu ya CCM wakati wa uchaguzi mkuu wa 2005, inaweza kutekelezeka. Wamesema, kamwe sera hiyo haitatekelezeka kwa kuwa Watanzania walio wengi hawajawezeshwa kuwa na ‘maisha bora’, sio tu kwa minajili ya kisiasa, lakini pia, katika fikra zao. Bado, wamesema, Watanzania walio wengi wana mtazamo kwamba maendeleo yao yanapaswa kuletwa na Serikali, bila kutambua kwamba ‘Serikali’ ni wao wenyewe, na si mamlaka fulani iliyoundwa kwa manufaa ya ‘wakoloni weusi’. Wamesema, kaulimbiu ya ‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania’ imekuwa hadaa kwani, licha ya kwamba haitekelezeki, waliobuni kauilimbiu hiyo hawakuwa na nia thabiti ya kuona kwamba inatekelezwa. Wamesema haya yanatokea kwa sababu milango ya kisiasa imefungwa kabisa kwa Watanzania walio wengi, kutokana na ukweli kwamba Watanzania walio wengi, kwanza, ‘wamefundishwa’ au ‘wamezoeshwa’ kuwapigia kura watu ambao ‘wananunua’ kura zao, kwa zawadi za khanga, vitenge, fulana, kofia, mchele, sukari, pilau, na fedha taslimu, wakati wa kampeni za uchaguzi. “Mtu asiyekuwa na uwezo wa kununua kura za Watanzania maskini hatachaguliwa, kwa kuwa Watanzania walio wengi wamezoea kununuliwa wakati wa uchaguzi… usipotoa takrima huchaguliwi,” walisema. Kwa mtazamo huo, wamesema kwamba kuipiga vita rushwa na kuitokomeza ni ndoto ya mchana, aghalabu, ndoto ya Alinacha au hekaya ya Abunuwasi, kwa hiyo wanaodai kwamba kuna jitihada au azma ya kuitokomeza rushwa waache ‘miyeyusho’, na kukubali kwamba bila Watanzania kuwezeshwa, kwa kila hali, kuanzia kwenye fikra zao, rushwa haitaondoka hapa nchini, na nafasi za uongozi wa kisiasa zitabakia kwenye himaya ya kundi la Watanzania wachache, waliobatizwa jina la ‘wakoloni weusi’. Kwa kuhitimisha ngwe hii, Watanzania wenzangu walisema, “Heri angekuwapo mkoloni, wote tungekuwa kwenye kundi moja, tungejua nani wa kulaumiwa… lakini kwa sasa, hali ilivyo, hata tukimlaumu mtu yeyote, ifikapo wakati wa uchaguzi, hali ni ile ile. Bado hatuoni faida ya uhuru huu!”

Kijamii: Hapa nilipata maoni mengi kiasi kwamba machozi ya uchungu yalinitiririka usoni, nikigundua kwamba binafsi nina ahueni kubwa mno kuliko Watanzania wenzangu wengi sana, ambao wako kwenye lindi la ufukara… si umaskini. Binafsi mimi ni maskini, si tajiri, ingawa ninaweza kuhesabiwa utajiri na hao mafukara. Lakini kiuchumi, mimi bado ni maskini.

Tukiangalia hali ya kijamii, Watanzania walio wengi wanaishi kwenye maeneo ambayo huduma za kijamii hupatikana katika hali iliyo chini ya kiwango kinachotakiwa, aghalabu, huduma hizo zikipatikana, ni kwa taabu isiyohesabika. Watanzania walio wengi wanaishi kwenye maeneo ambayo upatikanaji wa huduma za maji, umeme, shule, hospitali, masoko, utawala wa kiserikali, ni mgumu. Wanaoathirika zaidi na hali hii ni wanawake na watoto, wengi wao wakilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji, kuni, na kadhalika. Mifugo yao – kwa jamii za wafugaji – hulazimika kutembea umbali mrefu, kutafuta majani na maji kwa ajili ya lishe ya mifugo hiyo, jambo ambalo linasababisha uharibifu wa mazingira, kutokana na kutokuwapo kwa mipango ya ufugaji wa kisiasa. Kutokana na uduni wa hali ya kimaisha, wataalam wa ugani wa kilimo na mifugo hukataa kuwatembelea Watanzania wanoishi kwenye vijiji, jambo ambalo linachangia kuendelea kudumisha hali hiyo. Pale ambapo wataalam hawa wanakubali kwenda kuwajibika, wanawajibika kwa kiwango ambacho hutoa mchango mdogo ambao hauchangii katika maendeleo endelevu ya wananchi. Watanzania walio wengi, takriban asilimia 75, wanaishi kwenye makazi ambayo si bora kwa binadam, jambo ambalo linachangia kuendelea kuwapo kwa maradhi ambayo, pengine, yangeweza kuzuilika iwapo Watanzania hao wangewezeshwa kuishi kwenye makazi bora. Katika karne hii ya ishirini na moja, si jambo la ajabu kuona watu wakiishi kwenye nyumba zilizojengwa kwa udongo na miti na kuezekwa kwa nyasi, nyumba ambazo, dhahiri, hazifai kwa maisha bora ya binadam. Lakini nyumba hizi zipo, si jambo linalofichika kirahisi. Atakayekataa kuwapo kwa nyumba hizi ataonekana mtu wa ajabu na mnafiki wa kutupwa!

Kiuchumi: Hapa mwandishi wenu niliomba kupewa kitambaa cha kupenga makamasi kutokana na kilio cha kwikwi. Binafsi, hata nikilipwa shilingi milioni moja kwa mwezi, haitanitosha. Ninashangaa jinsi ambavyo ninaambiwa kuna Watanzania wanaoishi kwa kiwango au chini ya kiwango cha dola moja ya Marekani kwa siku! Dola moja? Ndio! Dola moja! Sithubutu hata kuchambua matumizi hayo, kwani hesabu zitanishinda!

Watanzania hawa ni wale ambao hawana uhakika wa kupata mlo mmoja wa uhakika kwa siku, sembuse wale ambao wana nafasi ya kupata milo mitatu, kwenye baadhi ya vijiji vichache sana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hawa ni wale mafukara, ambao Mungu peke yake ndiye anayewapa nguvu na uvumilivu wa kuendelea kuishi, pasi na kudadisi au kudai utekelezaji wa ahadi za uchaguzi, kisiasa zinavyoitwa ‘ilani za uchaguzi’, kutoka kwa wale waliowapa dhamana ya kuwawakilisha kwenye ngazi za juu za kitawala… Wabunge wao!

Mafukara wa Kitanzania wana umaskini wa makundi matatu; umaskini wa kifikra, umaskini wa fedha na umaskini wa kuwakilishwa kisiasa. Kutokana na kutokuwa na uwezo wa kifedha, elimu yao ni duni; hawapati elimu ya kuwawezesha kudadisi na kudai haki zao. Kutokana na umaskini wa kifikra, ambao unachangiwa na kuwa na viwango duni vya elimu, hawawezi kamwe kuwa na fikra za kimapinduzi, ambazo zingewawezesha kujipanga vizuri na kuamua kwa dhati mikakati yao kisiasa, kujiwekea mitazamo na mipango, pamoja na vigezo ambavyo wangevitumia kuwachagua wawakilishi wao Bungeni. Umaskini wa kifikra unawasababisha kukosa upeo wa kuchambua ‘chuya’ na ‘pumba’ kwenye mchele; kila ahadi inayoletewa mbele yao huonekana lulu au asali ya nyuki wadogo. Kibaya zaidi, kutokana na kuwa na umaskini wa uwakilishi wa kisiasa – kwa kuwa ni nadra sana, na kwa Tanzania jambo hili bado halijatokea, kwa mtu maskini kuchaguliwa kuwa Mbunge, Diwani, n.k. – wale ambao wamechaguliwa kuwawakilisha mafukanara hawa huwasahau mara tu wanaopoingia kwenye ‘kasri kubwa’ (Bunge) la watawala. Umaskini wa kisiasa ni mbaya zaidi, kwa kuwa mpaka sasa, hata vigezo vya uwakilishi vilivyotungwa na watawala, vinawabagua maskini hawa, kutokana na kukosa sifa ya kuwa na viwango vya elimu vinavyotakiwa, kama stashahada, shahada, vyeti, vyote hivi vikiwa ni sifa za uzoefu wa fani mbali mbali za kijamii, kisayansi na/au kiuchumi. Ni nadra pia kumpata ‘mtoto wa maskini’ akapata – licha ya kuwa na vigezo vya elimu vinavyohitajika – nafasi ya kuchaguliwa kwa kura, na kuwa mwakilishi wa ngazi ya Ubunge, Udiwani, n.k. Kama ‘watoto wa maskini’ wamechaguliwa, na wapo, ni wachache sana kuweza kuleta mabadiliko ya kweli kwa mafukara wenzao. Mara nyingi, ‘watoto wa maskini’ wanaobahatika kuchaguliwa kuwa wawakilishi ‘huzibwa mdomo’ kwa, ama zawadi au vitisho, pindi wanapojaribu kusimama kidete na kutetea ahadi zao walizozitoa wakati wa uchaguzi.

Ndugu Watanzania, haya ni maoni ya Watanzania wenzenu wachache, ambao wamenituma niwawakilishe, maoni haya yakiwa ni tafakuri zao kuhusu mustakabali wa Watanzania wote, baada ya miaka 46 ya Uhuru!

Watanzania hawa waliotoa maoni yao wamesema hawaoni sababu ya kusheherekea Uhuru kwa kuwa hawajanufaika na Uhuru huo; hali zao kimaisha zinaendelea kuwa duni, wakati kuna kundi la wachache linaloendelea kujineemesha siku hadi siku, mwaka hadi mwaka. Watanzania hawa wanadai kwamba wamelazimika kukimbilia kwenye miji mikubwa kwa kuwa angalau sehemu hizi zina unafuu wa maisha, kutokana na kuwa na nafasi nyingi zaidi za ajira, angalau hata kwa kibarua. Wamesema huko walikotoka ni kama vile wamesahauliwa, kwani maendeleo huja kwa msimu, kwa mfano kupitia miradi ya ujenzi wa miundombinu kama vile barabara. Ajira za msimu haziwasaidii, kwani, umaskini umechangia uharibifu wa mazingira; vyanzo vya maji vimeharibiwa na mifugo pamoja na Watanzania, mafukara wenzao, ambao wamefyeka misitu katika kujitafutia kipato kwa kuchoma mkaa, nishati duni ya kupikia.

Watanzania hawa wanasikitika kuwakimbia wenzao waliowaacha vijijini, lakini wanasema kwamba wale ambao wanaishi kwenye unafuu, huku mijini, wasisahau kwamba wana deni kwa wale ambao wana hali duni. “Wenzetu huko vijijini hawana amani, kwa sababu hawana uhakika wa kupata japo mlo mmoja kwa siku… wanaweza kukaa hata siku tatu bila kula mlo wa uhakika… wanashindia matunda, maziwa, mizizi, chochote kile… wakipata mlo mmoja siku hiyo kwano ni sherehe!” walisema. “Lakini tusijisahau, iko siku watakuja kutudai… iko siku…” walitahadharisha.

Kana kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa anasikiliza kilio cha Watanzania hawa, ambao walipata fursa ya kuwakumbuka wenzao wanaoishi vijijini, kwenye eneo la Mbezi kwa Yusufu, jijini Dar es Salaam, lori ambalo lilikuwa linasafirisha mafuta ya dizeli kuelekea jiji la Mwanza lilipata ajali na kuanguka kando kando ya barabara kuu ya Dar es Salaam-Morogoro, kupitia Kibaha na Chalinze. Kutokana na umaskini wao, watu wengi walipata fursa ya kuchota mafuta hayo ya dizeli, wakimtishia dereva wa lori hilo, ambaye alilazimika kukimbilia Polisi kusalimisha uhai wake. Takriban lita 200 za dizeli zilichotwa na watu wambao walikimbilia kwenye eneo hilo la ajali, wakiwemo wanaume, watoto, wanawake (hata wajawazito!), bila ya kutambua kwamba walikuwa wanahatarisha maisha yao, endapo mafuta hayo yangelipuka kwa moto wakati wowote ule! Ndio! Umaskini wa Watanzania wanaoishi kwenye Jiji la Dar es Salaam umewafanya wasahau kwamba kulikuwa na hatari ya moto, ambao ungewaka na kuwajeruhi wengi wao, pamoja na kuhatarisha maisha yao pia. Walichotambua ni kwamba, kulikuwa na nafasi ya kujichotea mafuta ya dizeli ya bure, na kukimbia nayo majumbani mwao, bila ya kutambua hatari ya moto ambayo ingeweza kutokea. Umaskini unawafanya watu washindwe kutambua kwamba matendo yao, ya kujitafutia/kujipatia kipato, hata kama si kwa njia halali, yangeweza kuhatarisha maisha yao! Hii ndiyo hali halisi, baada ya miaka 46 ya Uhuru!

Wakati wa Uhuru, nchi kama vile Thailand, Singapore, Malaysia, na kadhalika, barani Asia, zilikuwa na hali duni kuliko Tanzania. Leo hii, nchi hizo, hususan Singapore, ni tajiri maradufu, na zina maendeleo ya kiwango kikubwa cha kimataifa, kuliko Tanzania!

Wao waliweza nini? Sisi tumeshindwa nini?

Advertisements

One response to “Miaka 46 ya Uhuru!

 1. Massanda O'Mtima

  Tuna kila sababu ya kusherehekea miaka 46 ya uhuru wa nchi yetu.
  Kwanza kabisa, uhuru maana yake ni kuwa na fursa ya kufanya maamuzi juu ya hatima yenu. Lakini pia katika kusherehekea tunapata fursa ya kugeuka na kutathmini safari ilivyokuwa – ugumu, machungu, fursa na changamoto mbali mbali zilizopo mbele yetu. Mwenye kusema hakuna sababu ya kuusherehekea uhuru wetu ni mtumwa. Ni yule au wale wenye kusema afadhali ya mkoloni.
  Lakini pili, ni kwamba, maendeleo ni hatua. Ukubwa wa hatua katika safari hii hutegemea mambo mengi k.v. elimu au utambunzi wa jamii katika masuala mbali mbali, utayari wa viongozi mnaowachagua katika kuipeleka nchi yenu mbele, uzalendo wa viongozi na wananchi, mazingira / miundo mbinu / raslimali, uchapaji kazi / nidhamu ya jamii katika uzalishaji mali hadi kufikia ziada na matumizi yake, n.k, n.k.
  Sina uhakika, kwa mfano, ni kwa kiasi gani wananchi wanelewa maana ya uchaguzi / demokrasia. Je, wanajua kuwa kalamu na karatasi za kura wanazokuwa wameshikilia ili kuamua ni nani wamchague kwa siri wakiwa katika chumba cha kupigia kura ndivyo venye mustakabali wa nchi hii? Je, wale ambao hawajiandikishi wala kufika katika vituo vya kupigia kura wanajua kwamba huwapa nafasi wale wasiofaa kuingia kwenye uongozi?
  Je, wananchi wanaohudhuria kwenye mikutano na wakashindwa kuhoji au wakawa na ushabiki wa kijinga, wanajua kwamba huwajengea viongozi wabovu imani kwamba mambo ni murua hadi kuwafanya wabweteke? Na wale ambao hawahudhurii kwenye mikutano, wanashirikije kwenye shughuli za kuhoji maovu yanayojitokeza kutokana na uongozi mbaya au kutoa ushauri wa njia mwafaka wenye kuwapeleka mbele?
  Je, wananchi wanashirikije katika kuzalisha mali na shughuli za maendeleo yao? Au wanasubiri maisha bora kwa kila Mtanzania vitandani au vijiweni?
  Wale wenye kuwahudumia wananchi wenzao, wanao moyo wa uzalendo na huruma kwa wale wanaowahudumia – wagonjwa mahospitalini, wanafunzi mashuleni, wakulima mashambani, wavuja jasho katika maeneo mbali mbali, n.k, n.k?
  Je raslimali za nchi yetu zinasimamiwa na kutumika kwa manufaa ya nchi na wananchi wake?
  Hatima ya nchi yetu iko mikononi mwetu. Kila mwananchi na kila mzalendo! Zindukeni! Fanyeni kazi kwa bidii. Lindeni raslimali za nchi hii kwa uzalendo. Kuweni wakali dhidi ya wale wenye kulitafuna hili li-nchi. Msiwape nafasi mafisadi kututafuna. Vinginevyo mifano ya nchi iliyotolewa hapo juu itakuwa ni matamanio yasiyo na mwisho!
  Je hampendi kujengea kizazi kijacho mahali pema pa kuwakumbuka na kuwajivunia? Je mnataka historia ije iwahukumu vipi?
  Mungu wetu na awe nasi sasa na hata mwisho!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s