Utawala Bora au Bora Utawala?

Gazeti la kila siku la “Nipashe”, toleo la Alhamis, Desemba 13, 2007, katika ukurasa wake wa kwanza, limechapisha habari za kusikitisha, kuhusu mwanamke aliyelazimika kujifungua ndani ya ofisi ya Kata ya Ilola, Wilaya ya Shinyanga. Kwa mujibu wa mwandishi wa habari hizo, mwanamke huyo alikuwa amewekwa ‘chini ya ulinzi’ kwa madai ya kutolipa mchango wa shule ya sekondari ya kata, muda wake wa kujifungua ulipofika aliomba ruhusa ya kwenda hospitali kupata huduma ya uzazi, lakini watendaji waliomkamata walikataa kata-kata kumruhusu, hali iliyosababisha mwanamke huyo kujifungua ndani ya ofisi hiyo, mbele ya wanaume, jambo lililomdhalilisha na kumvunjia utu wake, ikiwa ni pamoja na haki zake za kibinadam. 

Dhana ya utawala bora, kimsingi, huangalia utendaji wa kiserikali unaozingatia miiko na maadili yanayokwenda sambamba na kuheshimu na kulinda haki za binadam. Mtendaji yeyote wa Serikali ambaye, chini ya kivuli cha madaraka yake, anapokiuka miiko na maadili hayo, kwa mfano, kuwakamata raia wasiolipa michango mbali mbali na kuwaweka kizuizini (kusema chini ya ulinzi ni kutumia lugha ya kidiplomasia…), hatimaye madhara kama yaliyotokea Ilola kutokea, mtendaji huyo anapaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu achilia mbali hatua za kisheria.

Lakini kwa wakati huu, ambao kiinimacho kinachotangazwa na Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kinaendelea kushangaza, kwani, badala ya kutueleza ni wapi fedha nyingi – zilizofikia kiwango cha trilioni – zinacopatikana na malipo ya kodi mbali mbali, zinakwenda wapi, Serikali hii inawahimiza raia wake kuchanga michango hiyo ya ujenzi wa shule za sekondari za kata.

Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005, CCM ilitoa ahadi kwamba Serikali itajenga shule za sekondari kufidia pengo la uhaba wa nafasi mpya za wanafunzi wa sekondari kutokana na wahitimu wengi waliokuwa wakimaliza shule za msingi kukosa nafasi ya kuendelea na sekondari. Hata hivyo, Serikali ya Awamu ya Nne haikusema ingejenga shule hizo za sekondari, zikiwamo za kata, kwa njia gani. Kilichotarajiwa ni kwamba, makusanyo makubwa ya kodi – ahadi nyingine iliyowekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi – yangechangia katika ujenzi huu wa shule za sekondari, kwani, Serikali imekiri kwamba inakusanya trilioni kadhaa za kodi kila mwaka kwa wakati huu.

Alipoanza kampeni yake ya ujenzi wa shule za sekondari za kata katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa Abbas Kandoro alisisitiza michango hiyo kutolewa kwa hiari, jambo ambalo wakazi wengi wa mkoa huu wamelipokea kwa dhati, na michango hiyo inaendelea kutolewa. Lakini kinachostaajabisha, kwa Watanzania waliopo nje ya mkoa huu, agizo lililotolewa kwenye Wizara ya Nchi – Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (TAMISEMI), ni kwamba, watendaji, wakiwamo maafisa watendaji wa kata, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, na kadhalika, wameamrishwa kukusanya fedha za ujenzi wa shule hizo za sekondari za kata kwa njia yoyote ile, zikiwamo kuwaswaga wananchi kama ng’ombe, kuwalazimisha kushughulika – watendaji hao wakisema ni ‘kujitolea’ – katika shughuli za ujenzi wa shule hizo, pamoja na kutoa michango ya lazima… hakuna hiari tena!

Jambo ambalo ‘watawala’ wetu wamekataa kukubali ni kwamba hali ya kiuchumi kwenye mikoa, hususan kwenye ngazi ya vijiji, ni ya umaskini na umaskini uliokithiri hadi kufikia ufukara. Asilimia kubwa ya Watanzania wanaoishi kwenye vijiji hawana uhakika wa kupata mlo mmoja kwa siku, huishia ‘kula’ matunda, muhogo wa kuchemsha, viazi vitamu, na vitu vyovyote vile wanavyoweza kuvipata ambavyo vinaweza kutumika kama ‘chakula’. Hawa ni watu ambao kuiona noti ya Shilingi 10,000/= ni jambo la nadra sana, sembuse noti ya Shilingi 1,000/=! Hawa ni watu maskini; unapowaambia watoe michango ya ujenzi wa shule za kata, kwa lazima, unawaweka kwenye hali ngumu, kwani, hawana vyanzo vya fedha kama Watanzania wengine (sio wengi…) wanaoishi kwenye miji midogo na mikubwa. Watu hawa wanapolazimishwa kuchangia huku hawana vyanzo vya fedha hata za kujikimu wao wenyewe, wanaowaagiza wafanye hivyo wanataka wakaibe ndipo wapate fedha hizo, au wazitoe wapi? 

Mama wa kijijini, tena mama mjamzito, ambaye hana kazi inayomwingizia kipato cha uhakika, anayemtegemea mumewe (kama ameolewa au mume wake yu hai…), anapoamrishwa kutoa mchango wa lazima, mama huyu hana uwezo wa kukataa wala kukubali, kwa sababu hana kipato. Lakini kutokana na ‘amri’ inayotoka kwa ‘wakubwa’, ambao nao wamepewa ‘amri’ ya kutimiza ‘malengo’, mama huyu anaishia kudhalilishwa na kuvunjiwa utu wake, pamoja na haki zake za kibinadam kukiukwa, kwa kulazimishwa kujifungua mbele ya hadhara ya wanaume, kana kwamba mama huyu si binadam tena, bali ni sawa na mnyama. Hata wanyama wanaofugwa huzaa watoto wao wakiwa mashambani, mabandani, au sehemu ambazo hakuna binadam wengi… wana nafuu zaidi. 

Ingawa uongozi wa juu wa mkoa wa Shinyanga umeunda tume ya kuchunguza hali iliyotokea katika Kata ya Ilola, binafsi sitarajii kwamba tume hiyo itapendekeza kuchukuliwa hatua zozote za kisheria kuchukuliwa dhidi ya Afisa Mtendaji wa Kata, kwa kuwa afisa huyo alikuwa akitimiza wajibu wake kikazi na kisheria. Hapa hatuzungumzii tena haki za kibinadam zilizokiukwa wakati wa kumweka kizuizini mama mjamzito, wala hatuzungumzii udhalilishaji aliofanyiwa mtu huyu maskini. Hatungepata nafasi ya kuzungumza juu ya tukio kama hili kufanyiwa mtu tajiri, kwani, mtu tajiri – hata mwanamke mjamzito – anao uhuru wa kuchagua, kuchangia ama kutochangia, na asifanywe lolote! 

Cha kushangaza, viongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne wanapanda majukwaani kila siku, wakihimiza utendaji bora wa kanuni za utawala bora, pamoja na kuadhimisha Siku ya Maadili Duniani, huku wakitoa maagizo yanayokiuka kanuni wanazozitetea. Unafiki wa ajabu na wa kutisha! 

Huu ni Utawala Bora au Bora Utawala?

Advertisements

One response to “Utawala Bora au Bora Utawala?

  1. Natoa pole sana kwa huyu mama kuzailishwa namna hiyo kwa kuzaa mbele za hao wanaume, baada ya tume kuka imefikia wapi ningependa kujuatukio hili liliishiaje. Pole mama mzazi.

    Nadhali, watu wangejaribu kuwa wanadamu na si vinginevyo, kama mtu anaonyesha kabisa hali yake na uwezo hakuwa nao walitaka atoe nini???
    Nadhani mama huyu alidhalilishwa sana. Hebu tutangulize Utu kwanza halafu pesa baadae. Kweli Upendo wa wengi umepoa. Uongozi bora ni kutafuta mbinu za kuwafanya watu wawe na miradi gani ili zipatane pesa kutokana na miradi ziweze mfano kujengea shule. Je? sasa Ilola kuna shule ngapi za sekondari zilizofunguliwa?Wewe kiongozi hebu ongoza watu kwa kutumia kanuni za uongozi bora. Naomba uhifadhi jina na email yangu tafadhali.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s